Thursday, 7 September 2017

CCM yatoa tamko kuhusu lissu kupigwa risasi

CCM Yatoa Tamko Tundu Lissu Kupigwa Risasi
11 hours ago

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole kimelaani kitendo alichofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kwa kupigwa risasi leo mchana nyumbani kwake Dodoma.

Taarifa hiyo ya CCM inalaani kitendo hicho cha kikatili na kusema si kitendo cha utu hivyo kimelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwachukulia sheria kali wote ambao watapatikana kuhusika katika tukio hilo. 

Rais Magufuli awataka wateule wake wajitumbue wenyewe

Breaking News: Rais Magufuli Amtaka Simbachawene na Wenzake WAJITUMBUE Wenyewe
17 hours ago
Rais Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wa serikali ambao wametajwa kwenye ripoti za bunge ya madini ya Almasi na Tanzanite wamepishe nafasi zao ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri kuwachunguza.

Rais Magufuli amesema hayo leo wakati akikabidhiwa ripoti hizo Ikulu jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kusema amesikia baadhi ya viongozi mbalimbali wengine ambao amewateuwa yeye kuwa wameusishwa kwenye wizi huo hivyo amewataka wapishe.

"Wako watu wametajwa tajwa, na wengine mimi ndio nilihusika kuwateua sasa ukishatajwa tajwa, naagiza vyombo vya ulinzi na usalama vifuatilie hili tena kwa haraka.

" Wale ambao wametajwa tajwa kwenye ripoti hii ambao ni wateule wangu, ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri, ni matumaini yangu watakaa pembeni"alisema Rais Magufuli


Katika ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa jana mjini Dodoma na leo kukabidhiwa kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa iliweza kuwataja baadhi ya viongozi wa serikali ikiwepo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. George Simbachawene, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Jinsi Tundu lissu alivopigwa risasi

Mbunge wa Rombo Asimulia Jinsi Tundu Lissu Alivyopigwa Risasi
10 hours ago
Mbunge wa Rombo, Joseph  Selasini ameeleza jinsi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alivyopigwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.

Selasini amesema kuwa maelezo aliyopata ni kuwa alikuwa akifuatiliwa na  gari tangu anatoka bungeni na dereva wake alilishtukia.                     

Amesema kuwa alivyoona wanamfutilia alipofika nyumbani, dereva alimsihi Lissu asishuke ndani ya gari.                      

"Hao watu walipoona hawashuki walijifanya kuna kitu wanaangalia walivyoona kuna utulivu walisogeza gari lao ambalo ni tinted na kuanza kurusha risasi upande wa Lissu." amesema                     

Selasini amesema, “Risasi zilimpata mguuni, mkononi na tumboni lakini daktari anasema anaendelea vizuri."

Lissu amepigwa risasi leo Alhamisi  na kupelekwa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Wanasheria TLS waja na tanko hili


10 hours ago
Sisi Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tangangika (Tanganyika Law Society, TLS) tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa tukio la Rais wa chama chetu, Mh. Tundu Lissu, kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake huko Dodoma leo hii mchana. Taarifa tulizo nazo mpaka sasa ni kwamba Mh Tundu Lissu bado yupo hospitali kuu ya Dodoma akipatiwa matibabu ya dharura. Tunamuomba Mungu azidi kumlininda na kumhifadhi Mh Tundu Lissu.

Kwa vyovyote vile, hivi sasa bado ni mapema sana kujua ni nani hasa wahusika wa tukio hili la kinyama na dhamiri yao, lakini, kwa niaba yetu na wanachama wetu, mawakili wa Tanganyika, tunalaani na kukemea vikali kitendo hiki cha kihalifu na cha uoga mkubwa.

Wito wetu kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni kwamba wafanye kazi yao kwa umakini, haki na weledi ili kuwapata watu waliofanya unyama huu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Sisi kwa upande wetu tunalifuatilia suala hili kwa ukaribu, na tutaendelea kuufahamisha umma kinachoendelea.

Mwisho, tunatoa pole kwa familia ya Mh. Tundu Lissu, ndugu na jamaa zake, wanachama wetu wa Chama cha Mawakili Tanganyika na watanzania wote ambao wameguswa na tukio hilo. Tunaomba kila mmoja wetu kwa imani yake amuombee ndugu yetu Mh Tundu Lissu apone na apate nafuu haraka ili tuungane naye tena katika shughuli zetu za kila siku.
Tunawaomba wanachama na watanzania wote waendelee kuwa wavumilivu na watulivu wakati huu. Na kuujumla wetu tulaani na kukemea kitendo hiki ambacho hakikubaliki katika mila na desturi zetu kama Taifa.
Ahsanteni.

Imetolewa na
Godwin Simba Ngwilimi (Wakili), Makamu wa Rais, TLS,
Kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)

Dar es Salaam

CHADEMA YATEMA CHECHE,TUNDU LISSU MAHUTUTI

Chadema yatoa Tamko Tundu Lissu Kupigwa Risasi
10 hours ago
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa mshtuko taarifa ya kupigwa risasi mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, amepigwa risasi baada ya kikao cha Bunge mchana wa leo Alhamisi.

Shambulio hilo limetokea leo mchana nyumbani kwa Lissu, Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

“Chadema tunalaani vikali kitendo hicho na tunafuatilia kwa karibu hali yake,” imesema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Uenezi, Mawasiliano na Mahusiano ya Nje ya Chadema makao makuu.

Wakati huohuo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema umepokea kwa mshtuko taarifa za kupigwa risasi Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Mratibu wa mtandao huo,  Onesmo ole Ngurumwa katika taarifa amesema wanatoa pole kwa familia ya Lissu, wananchi wa Singida Mashariki, wanachama wa TLS na Watanzania kwa jumla.

Mtandao huo umewahimiza Watanzania wote kumwombea Lissu.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako Lissu anaendelea na matibabu.                      

Pia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amefika hospitalini hapo ambako Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Charles amesema Lissu yu hai na imara.

Dk Charles akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita amesema mbunge huyo amepigwa risasi tumboni na kwamba timu ya madaktari inaendelea na matibabu.

Rais Magufuli ampa pole tundu lisu

Rais John Magufuli, amesema amepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli amesema anamuombea Lissu kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka.

“Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria,” amesema.

Lissu amejeruhiwa leo Alhamisi mchana akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.