Thursday, 7 September 2017

CCM yatoa tamko kuhusu lissu kupigwa risasi

CCM Yatoa Tamko Tundu Lissu Kupigwa Risasi
11 hours ago

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole kimelaani kitendo alichofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kwa kupigwa risasi leo mchana nyumbani kwake Dodoma.

Taarifa hiyo ya CCM inalaani kitendo hicho cha kikatili na kusema si kitendo cha utu hivyo kimelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwachukulia sheria kali wote ambao watapatikana kuhusika katika tukio hilo. 

Rais Magufuli awataka wateule wake wajitumbue wenyewe

Breaking News: Rais Magufuli Amtaka Simbachawene na Wenzake WAJITUMBUE Wenyewe
17 hours ago
Rais Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wa serikali ambao wametajwa kwenye ripoti za bunge ya madini ya Almasi na Tanzanite wamepishe nafasi zao ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri kuwachunguza.

Rais Magufuli amesema hayo leo wakati akikabidhiwa ripoti hizo Ikulu jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kusema amesikia baadhi ya viongozi mbalimbali wengine ambao amewateuwa yeye kuwa wameusishwa kwenye wizi huo hivyo amewataka wapishe.

"Wako watu wametajwa tajwa, na wengine mimi ndio nilihusika kuwateua sasa ukishatajwa tajwa, naagiza vyombo vya ulinzi na usalama vifuatilie hili tena kwa haraka.

" Wale ambao wametajwa tajwa kwenye ripoti hii ambao ni wateule wangu, ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri, ni matumaini yangu watakaa pembeni"alisema Rais Magufuli


Katika ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa jana mjini Dodoma na leo kukabidhiwa kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa iliweza kuwataja baadhi ya viongozi wa serikali ikiwepo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. George Simbachawene, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Jinsi Tundu lissu alivopigwa risasi

Mbunge wa Rombo Asimulia Jinsi Tundu Lissu Alivyopigwa Risasi
10 hours ago
Mbunge wa Rombo, Joseph  Selasini ameeleza jinsi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alivyopigwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.

Selasini amesema kuwa maelezo aliyopata ni kuwa alikuwa akifuatiliwa na  gari tangu anatoka bungeni na dereva wake alilishtukia.                     

Amesema kuwa alivyoona wanamfutilia alipofika nyumbani, dereva alimsihi Lissu asishuke ndani ya gari.                      

"Hao watu walipoona hawashuki walijifanya kuna kitu wanaangalia walivyoona kuna utulivu walisogeza gari lao ambalo ni tinted na kuanza kurusha risasi upande wa Lissu." amesema                     

Selasini amesema, “Risasi zilimpata mguuni, mkononi na tumboni lakini daktari anasema anaendelea vizuri."

Lissu amepigwa risasi leo Alhamisi  na kupelekwa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Wanasheria TLS waja na tanko hili


10 hours ago
Sisi Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tangangika (Tanganyika Law Society, TLS) tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa tukio la Rais wa chama chetu, Mh. Tundu Lissu, kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake huko Dodoma leo hii mchana. Taarifa tulizo nazo mpaka sasa ni kwamba Mh Tundu Lissu bado yupo hospitali kuu ya Dodoma akipatiwa matibabu ya dharura. Tunamuomba Mungu azidi kumlininda na kumhifadhi Mh Tundu Lissu.

Kwa vyovyote vile, hivi sasa bado ni mapema sana kujua ni nani hasa wahusika wa tukio hili la kinyama na dhamiri yao, lakini, kwa niaba yetu na wanachama wetu, mawakili wa Tanganyika, tunalaani na kukemea vikali kitendo hiki cha kihalifu na cha uoga mkubwa.

Wito wetu kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni kwamba wafanye kazi yao kwa umakini, haki na weledi ili kuwapata watu waliofanya unyama huu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Sisi kwa upande wetu tunalifuatilia suala hili kwa ukaribu, na tutaendelea kuufahamisha umma kinachoendelea.

Mwisho, tunatoa pole kwa familia ya Mh. Tundu Lissu, ndugu na jamaa zake, wanachama wetu wa Chama cha Mawakili Tanganyika na watanzania wote ambao wameguswa na tukio hilo. Tunaomba kila mmoja wetu kwa imani yake amuombee ndugu yetu Mh Tundu Lissu apone na apate nafuu haraka ili tuungane naye tena katika shughuli zetu za kila siku.
Tunawaomba wanachama na watanzania wote waendelee kuwa wavumilivu na watulivu wakati huu. Na kuujumla wetu tulaani na kukemea kitendo hiki ambacho hakikubaliki katika mila na desturi zetu kama Taifa.
Ahsanteni.

Imetolewa na
Godwin Simba Ngwilimi (Wakili), Makamu wa Rais, TLS,
Kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)

Dar es Salaam

CHADEMA YATEMA CHECHE,TUNDU LISSU MAHUTUTI

Chadema yatoa Tamko Tundu Lissu Kupigwa Risasi
10 hours ago
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa mshtuko taarifa ya kupigwa risasi mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, amepigwa risasi baada ya kikao cha Bunge mchana wa leo Alhamisi.

Shambulio hilo limetokea leo mchana nyumbani kwa Lissu, Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

“Chadema tunalaani vikali kitendo hicho na tunafuatilia kwa karibu hali yake,” imesema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Uenezi, Mawasiliano na Mahusiano ya Nje ya Chadema makao makuu.

Wakati huohuo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema umepokea kwa mshtuko taarifa za kupigwa risasi Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Mratibu wa mtandao huo,  Onesmo ole Ngurumwa katika taarifa amesema wanatoa pole kwa familia ya Lissu, wananchi wa Singida Mashariki, wanachama wa TLS na Watanzania kwa jumla.

Mtandao huo umewahimiza Watanzania wote kumwombea Lissu.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako Lissu anaendelea na matibabu.                      

Pia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amefika hospitalini hapo ambako Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Charles amesema Lissu yu hai na imara.

Dk Charles akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita amesema mbunge huyo amepigwa risasi tumboni na kwamba timu ya madaktari inaendelea na matibabu.

Rais Magufuli ampa pole tundu lisu

Rais John Magufuli, amesema amepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli amesema anamuombea Lissu kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka.

“Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria,” amesema.

Lissu amejeruhiwa leo Alhamisi mchana akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Thursday, 24 August 2017

TUNDU LISSU AACHIWA KWA DHAMANA

Ndani ya mahabusu kwa saa 48 hatimaye Mwanasheria Mkuu wa Chama na rais wa TLS Mh Tundu Lissu amepewa dhamana ya Polisi majira ya saa 11 jioni.

Amepewa masharti ya kuripoti kituo cha polisi Jumatatu tarehe 28/8/2017 wakati wowote akiwa na muda.

Amedhaminiwa na mawakili wake Fred Kihwelo na Msemo.

MATUMIZI SAHIHI YA MANENO HAPANA,NDIYO NA LABDA

Leo tunakwenda kuangalia maneno matatu muhimu, ambayo huwa tunayatumia kirahisi, lakini madhara yake ni makubwa. Tukijua namna sahihi ya kutumia maneno haya, tutaweza kufanya mapinduzi makubwa sana kwenye maisha yetu.
Maneno tunayokwenda kuyaangalia leo ni NDIYO, HAPANA na LABDA.
Haya ni maneno ambayo yanahusiana moja kwa moja na matumizi ya muda wetu. Kuna namna sahihi ya kutumia maneno haya ambayo inatuwezesha kuwa na muda wa kutosha kufanya mambo muhimu kwetu. Pia ipo namna ambayo siyo sahihi ya kutumia maneno haya, na inatupelekea kupoteza muda mwingi kwenye maisha yetu.
Neno NDIYO.
Hili ni neno ambalo tumekuwa tunalitumia vibaya kwenye maisha yetu, ni neno moja ambalo limekuwa linapoteza muda wetu kuliko maneno mengine yoyote.
Kwa mfano umepanga kwamba kila siku jioni unapomaliza kazi zako, utakuwa unasoma kitabu ili kuongeza maarifa zaidi ya kile unachofanya. Umefika muda na umekaa kuanza kusoma kitabu chako, mara inaingia simu ya rafiki yako, anakuambia yupo sehemu fulani na marafiki wengine, na wanakuulizia. Wewe unasemaje, NDIYO, nakuja. Na unajipa sababu kabisa kwamba nisipoenda watanichukuliaje, hichi kitabu naweza kukisoma muda wowote tu.
Hilo ni moja, lakini yapo mengi sana tunayosema ndiyo ambayo yanatupotezea muda wetu. Mambo kama simu, ujumbe wa simu, mitandao ya kijamii, habari, umbeya na mengine mengi, tunaposema ndiyo kuyafuatilia, maana yake tunahamisha matumizi ya muda wetu. Tunaacha kufanya yale ambayo ni muhimu sana kwetu, na kuishia kufanya yale ambayo siyo muhimu.
Watu wengi husema ndiyo kwa sababu wanaogopa kusema hapana. Wanaona wakisema hapana wanawaumiza wengine na hivyo kukubali ili tu kuwaridhisha. Na nataka nikuambie leo rafiki yangu, hakuna sababu ya hovyo ya kusema ndiyo kama hiyo. Na ni kwa sababu zifuatazo;
Moja; unaposema ndiyo kwenye mambo ya wengine, maana yake unasema hapana kwenye mambo yako binafsi. Hivyo kama unawaridhisha wengine, jua kabisa kwamba unajiangusha wewe mwenyewe.
Mbili; hakuna anayejali kuhusu wewe kama unavyofikiria. Usidhani kwamba watu muda wote wanafikiri kuhusu wewe pekee na namna umewakatalia kuhusu kitu fulani, watu wanaendelea na maisha yao.
Tatu; kusema ndiyo kwa sababu unaogopa kusema hapana, hakutakuacha salama. Kwa sababu hutakamilisha ndiyo ile kama ulivyoahidi na hapo utaharibu zaidi mahusiano yako na wale uliowaambia ndiyo. Unajua ni bora useme hapana watu watafute wengine wanaoweza kufanya, kuliko useme ndiyo halafu uanze kuwazungusha.
Neno HAPANA.
Hili ndiyo neno lenye uhuru kwako na maisha yako. Unaposema hapana, unajijengea uhuru, unajipa muda wa kufanya yale ambayo ni muhimu kwa maisha yako. Unaposema hapana, unajipa nafasi ya kuendesha maisha yako vile unavyotaka wewe.
Lakini neno hapana ni neno ambalo wengi wana hofu ya kulitumia. Wengi huona ni vibaya na kuona wengine watawachukulia vibaya, au wataonekana wana dharau kwa kusema hapana.
Na hapa ndipo sanaa inapohitajika, haimaanishi mtu akuombe kufanya kitu halafu umwambie HAPANA siwezi kufanya. Zipo njia nyingi za kusema hapana bila ya kuwaumiza wengine, lakini hapana ikawa imefika.
Kwa mfano mtu amekuomba uhudhurie kikao cha harusi, ambacho unajua hakuna kitu kikubwa mnakwenda kufanya pale, kwa sehemu kubwa ni kuongea mambo yale yale ambayo yamekuwa yanaongelewa, labda kukusanya michango. Unaweza kumwambia nashukuru sana kwa nafasi hii ya kushiriki kikao hicho, lakini kwa wakati huo wa kikao nina jambo jingine nafanyia kazi, nawatakia kila la kheri na kikao kiende vizuri.
Kwa vyovyote vile, hakikisha unasema hapana, na unaisema kwa namna ambayo mtu ataona ni sawa.
Je ni mambo gani useme hapana?
Kwako binafsi; jambo lolote ambalo halichangii wewe kufikia ndoto za maisha yako, sema hapana. Sema hapana kwa habari, udaku, majungu, umbeya, mitandao ya kijamii, uvivu na kufuatilia maisha ya wengine.
Kwa wengine; chochote ambacho mtu anataka ufanye, ambacho siyo muhimu sana kufanyika kwa wakati huo, na kinakuzuia wewe kufanya makubwa ziadi, sema hapana.
Neno LABDA.
Hili ni neno la hovyo kabisa, na usilitumie kabisa. Lifute kabisa kwenye orodha ya maneno unayotumia.
Watu wamekuwa wakitumia neno labda ili kukaa katikati ya ndiyo na hapana. Wanakuwa wanataka kusema hapana, lakini wanaogopa, na wakati huo hawapo tayari kusema ndiyo, hivyo wanasema labda.
Kutumia neno labda kutakuharibia mambo mengi kuliko unavyofikiri. Watu watakuchukulia kama mtu usiye na msimamo na usiyeeleweka. Kusema labda kunawafanya watu washindwe kujua unasimama wapi na wategemee nini kwako.
Sema NDIYO kwenye yale mambo muhimu, sema HAPANA kwa mambo ambayo siyo muhimu na kamwe usitumie neno LABDA.
Fanyia kazi haya rafiki, na matumizi ya muda wako yatakuwa bora sana.

NJIA ZA KUA KIONGOZI BORA

Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi sana, mambo mengi ambayo yalikuwa yamezoeleka sasa hivi hayana tena nafasi.
Mabadiliko haya ya kasi yanaleta changamoto kubwa kwa viongozi wa zama hizi. Wengi wameendelea kufanya mambo kwa mazoea na hivyo kushindwa au kukosa kabisa maarifa sahihi ya kuwa viongozi bora.
Mshauri wa mambo ya uongozi, Warreb Bennis, mwaka 1987 aliandika kitabu ON BECOMING A LEADER, akiangalia sifa za viongozi ambao wameweza kuwa na mafanikio makubwa. Miaka zaidi ya 20 baadaye, alitoa toleo jingine la kitabu hichi, kuonesha mabadiliko yanayoendelea duniani na namna viongozi bora wanavyokuwa viongozi bora.
Kupitia kitabu hichi, ametushirikisha misingi ambayo viongozi wenye mafanikio makubwa wamekuwa wanaiishi na imekuwa na msaada kwao.
Kwa sababu kila mmoja wetu anapaswa kuwa kiongozi kwa namba moja au nyingine, ni muhimu kila mmoja wetu akaijua misingi hii na kuitumia kwenye maisha yake ili kuweza kufanikiwa.
Karibu kwenye uchambuzi hii wa kitabu cha ON BECOMING A LEADER, nikushirikishe yale muhimu ambayo nimejifunza kwenye kitabu hichi. Mwisho kabisa nitakupa utaratibu wa kupata kitabu hichi ili uweze kukisoma zaidi.
  1. Uongozi wa zama hizi ni ushirikiano.
Zamani ilizoeleka kwamba kiongozi ndiyo mwenye majibu yote sahihi na watu walipaswa kumfuata pekee. Lakini zama hizi uongozi ni ushirikiano baina ya kiongozi na wafuasi. Dunia ya sasa ina changamoto nyingi na ngumu, hakuna mtu mmoja anayeweza kuzitatua yeye peke yake, ushirikiano ni muhimu mno.
Ili kuwa kiongozi bora, tengeneza ushirikiano baina yako na wale ambao unawaongoza, wajione sehemu ya timu na siyo tu watu wa kufuata amri. Kwa njia hii utapata ushirikiano mzuri na mawazo mazuri kutoka kwa wengine.
  1. Uhodari wa aina nne ambao viongozi bora wanao.
Kila kiongozi bora, ambaye ameweza kuwa na mafanikio makubwa, amekuwa na uhodari wa aina nne.
Moja; uwezo wa kuwashawishi wengine kupitia kile wanachofanya. Viongozi hawa wanakuwa na maono makubwa ambayo wengine wanahamasika kujiunga nao na kuweza kuyafikia kwa pamoja.
Mbili; wana sauti yao ya kipekee, ambayo wafuasi wanaikubali na kuifuata. Sauti hapa inahusisha vitu vingi, kusudi, kujiamini na ukomavu wa kihisia.
Tatu; uadilifu, viongozi wote wenye mafanikio wana uadilifu wa hali ya juu, wanayo misingi ambayo wanaiishi na kuisimamia. Maneno yao na matendo yao ni kitu kimoja.
Nne; utayari wa kubadilika, huu ndiyo uhodari wa tofauti zaidi kwa zama hizi za mabadiliko makubwa. Wale ambao wapo tayari kubadilika hata kama hawajawa tayari, wamekuwa viongozi bora.
Jijengee uhodari huu wa aina nne ili kuwa kiongozi bora.
  1. Kujifunza uongozi siyo kitu rahisi.
Watu wengi wamekuwa wanabishana iwapo viongozi wanazaliwa au wanatengenezwa (kufundishwa). Na mara nyingi imekuwa inaishia kwamba viongozi wanatengenezwa. Lakini unapoangalia kwa undani zaidi, unagundua siyo sahihi kwamba viongozi wanatengenezwa kwa kufundishwa, bali viongozi wanajitengeneza wenyewe.
Uongozi ni mgumu sana kiasi cha mtu kuweza kufundishwa. Hii ni kwa sababu uongozi unahusisha mambo mengi, na zaidi watu. Sasa unaweza kutabiri na kupangilia kila kitu, lakini siyo watu. Watu hawatabiriki.
Ili kuwa kiongozi bora, kuwa tayari kujitengeneza wewe mwenyewe kuwa kiongozi, na hatua ya kwanza kufanya hivyo ni kujijua wewe mwenyewe kwanza.
  1. Mkishakuwa watu watatu, uongozi ni lazima.
Mtu mmoja akiwa mwenyewe jangwani, hahitaji sana uongozi, anaweza kuendesha maisha yake namna anavyoweza. Mkiwa watu wawili, na kama mmeshibana sana, mnaelewana kwa kila jambo, mnaweza kwenda vizuri bila ya uongozi. Lakini mkishakuwa watatu, lazima mmoja awe kiongozi la sivyo hamtaweza kufanya chochote.
Kwa kuwa maeneo mengi ya maisha yako unakuwa na watu wengine, kuanzia kwenye familia mpaka kwenye kazi zako, ni muhimu sana uwe kiongozi bora.
  1. Sababu tatu kwa nini viongozi ni muhimu sana.
Moja; viongozi ndiyo wenye jukumu la ufanisi wa taasisi wanayoongoza. Kushinda au kushindwa kwa taasisi kunatokana na maamuzi ambayo kiongozi wa taasisi hiyo anayafanya.
Mbili; mabadiliko yanayoendelea kwa kasi yanahitaji kuwa na mtu wa kuweza kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajaleta madhara makubwa. Kwa sehemu kubwa kiongozi anapaswa kuliona hilo mapema.
Tatu; kila taasisi kwa zama hizi inapimwa kwa uadilifu wake, kiongozi wa taasisi ndiye anayewajibika kwa uadilifu wa taasisi yake, kulingana na namna anavyoiendesha, watu anaowapa nafasi na kazi zinavyofanyika.
  1. Maisha siyo njia iliyonyooka.
Kitu kikubwa kinacholeta changamoto kwenye uongozi ni kwamba maisha siyo njia iliyonyooka. Hakuna mipango ambayo inatokea kama ilivyopangwa. Hakuna hatua ambazo ukitoka moja unaenda nyingine. Mambo yanaweza kutokea kwa mpangilio ambao hata haueleweki. Bila ya kuwa na uongozi imara, taasisi inaweza kukosa uelekeo kwa mambo yanavyoenda zama hizi.
  1. Hatua nne za kiongozi kuweza kufanikiwa kwenye dunia isiyoeleweka.
Kwa kuwa dunia tunayoishi sasa haieleweki, mipango haiendi kama tulivyopanga, viongozi wanaofanikiwa wanapitia hatua hizi nne;
Moja; wanajijua wao wenyewe, kwa kujua wanaweza kufanya nini na hawawezi kufanya nini.
Mbili; wanasikiliza sauti iliyopo ndani yako, kila mtu ana sauti ya ndani, ila wengi wamekuwa hawaisikilizi.
Tatu; kujifunza kutoka kwa mamenta sahihi, viongozi wanaofanikiwa wana watu ambao wanajifunza kutoka kwao.
Nne; kuongozwa na maono makubwa, bila ya maono makubwa, kelele zilizopo zinawapoteza viongozi.
  1. Misingi mikuu ya viongozi wenye mafanikio.
Viongozi wapo wa kila aina na kila rangi, warefu, wafupi, weupe na weusi, vijana na wazee. Lakini wote wana misingi ambayo wanaifuata, misingi hiyo ni kama ifuatavyo;
Moja; wanaongozwa na maono makubwa, wanajua kabisa nini wanataka na kwa nini wanakitaka.
Mbili; mapenzi juu ya kile wanachofanya, haya ndiyo yanawasukuma kufanya.
Tatu; uadilifu ambao unahisisha maeneo matatu; kujitambua, uvumilivu na ukomavu.
Nne; uaminifu, ambalo ni zao la uadilifu.
Tano; udadisi na uthubutu, hii inawawezesha kugundua vitu vipya na kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajawasumbua.
  1. Viongozi siyo mameneja.
Kumekuwepo na tofauti nyingi kati ya viongozi na mameneja, lakini tofauti kubwa kabisa ni kwamba viongozi wanawawezesha watu kuwa bora zaidi huku mameneja wakiwasimamia watu. Tofauti nyingine ni kama ifuatavyo;
Mameneja wanasimamia, viongozi wanahamasisha.
Mameneja ni kopi, viongozi ni halisi.
Mameneja wanatunza hali kama ilivyo, viongozi wanaboresha hali iliyopo.
Mameneja wanakazana na mifumo na michakato, viongozi wanakazana na watu.
Mameneja wana mtazamo wa karibu, viongozi wana mtazamo wa mbali.
Mameneja wanauliza VIPI na LINI, viongozi wanauliza NINI na KWA NINI.
Mameneja wanakubaliana na mfumo kama ulivyo, viongozi wanabadili mfumo ili kuwa bora zaidi.
Mameneja wanafanya vitu kwa usahihi, viongozi wanafanya vitu sahihi.
Kuwa kiongozi, usiwe maneja.
  1. Udhaifu ndiyo unaamua uongozi.
Lipo jambo moja la kushangaza sana kwenye uongozi na tabia. Viongozi bora kabisa huwa wanafanikiwa licha ya kuwa na madhaifu fulani kwenye maisha yao. Lakini pia, viongozi wabaya huwa wanafanikiwa kwa kutumia madhaifu yao.
Hivyo kama usipoyajua madhaifu yako vizuri, yanaweza kukupelekea ukafanikiwa kama kiongozi mbaya kuwahi kutokea. Lakini kama utayajua vizuri, unaweza kufanikiwa kuwa kiongozi mzuri.
  1. Kazi kubwa ya kiongozi ni kujitengeneza yeye mwenyewe na kuiepuka jamii.
Jamii zetu huwa zinafanya kazi moja kubwa sana, kuhakikisha watu wote wanakuwa sawa. Kila mtu afanye kile ambacho kila mtu anafanya. Sasa ukienda na maisha hayo, kwa kufanya yale ambayo kila mtu anataka ufanye, huwezi kuwa kiongozi bora.
Ili uwe kiongozi bora lazima ujue ule utofauti uliopo ndani yako, lazima ujijue wewe mwenyewe vizuri. Lazima ujue maeneo gani uko vizuri na maeneo yapi una udhaifu, kisha kuchukua hatua ya kuwa bora zaidi.
  1. Kujitabua na kujitengeneza hakuna mwisho.
Tunapokuwa watoto, tunatengenezwa na jamii, tunapelekwa shule, tunafundishwa majumbani na hata kwenye jamii. Tunapokuwa watu wazima, ndipo kazi ya kujitengeneza sisi wenyewe inapoanza. Kwanza tunahitaji kuanza kujitambua, maana jamii haikutupa fursa hiyo. Baada ya kujitambua ndiyo tunajitengeneza kuwa bora zaidi.
Sasa hili la kujitambua na kujitengeneza halina umri maalumu kama yale malezi mengine ya kwenye jamii. Wengine hupata fursa ya kujitambua na kujitengeneza wakiwa na miaka 20, wengine mpaka wanafika miaka 50 wanakuwa bado hawajapata fursa hiyo. Na hata baada ya kujitambua, bado kujitengeneza kunaendelea, hakuna mwisho mpaka mtu anakufa.
  1. Masomo manne muhimu kwenye kujitambua.
Kwenye kujitambua, yapo masomo manne muhimu unayopaswa kuyajua na kuyafanyia kazi.
Moja; wewe ndiye mwalimu bora zaidi kwako. Hakuna mwalimu anayeweza kukufundisha zaidi ya unavyoweza wewe mwenyewe.
Mbili; kubali majukumu yako, usimlaumu mtu yeyote. Ukianza kuwalaumu na kuwalalamikia wengine kuhusu maisha yako, bado hujajitambua.
Tatu; unaweza kujifunza chochote unachotaka kujifunza. Kama bado unasema huwezi kwa sababu hujui kitu fulani, kwa nini usijifunze? Dunia ya sasa unaweza kujifunza mwenyewe kila kitu.
Nne; uelewa wa kweli unatokana na kutafakari uzoefu wako. Kila kitu ambacho umewahi kupitia kwenye maisha yako, kina maana na mchango kwa hapo ulipo sasa. Unahitaji kupata muda wa kutafakari maana ya kila kitu na namna kimekufikisha hapo ulipo sasa.
Fanyia kazi masomo haya manne, ili uweze kujitambua na kuwa kiongozi bora.
  1. Usichokielewa, siyo chako.
Kitu chochote ambacho hukielewi au hujakijua kwa undani, siyo chako. Hata wewe mwenyewe, kama bado hujajitambua, utaishia kutumiwa na watu wengine badala ya kujitumia wewe mwenyewe.
Unapaswa kuelewa kwa undani kila kinachohusiana na wewe, hapo ndipo unaweza kukitumia vizuri kwa mafanikio yako.
  1. Katika kujifunza, unapaswa pia kufuta uliyojifunza.
Mambo mengi uliyofundishwa shuleni na hata kufundishwa na wazazi, yanaweza kuwa kikwazo kwako katika kufanikiwa kwenye uongozi. Kwa mfano huenda umeaminishwa njia pekee ya kufanikiwa kwenye maisha ni kupata ajira ya aina fulani. Hili unaweza kuwa unaliamini kabisa, lakini wewe unapenda vitu tofauti na kazi unayofanya.
Hapa unahitaji kujifunza upya kwa kuanza kufuta yale ambayo umejifunza kwa muda mrefu. Kwa njia hii utaanza kuona ukweli kwamba maisha ni kile unachotengeneza wewe, na watu wote hatufanani.
  1. Wewe ni zao la kila kitu umewahi kukutana nacho kwenye maisha.
Kumekuwa na mabishano mengi, iwapo tabia za watu zinatokana na mazingira wanayoishi au ni za kurithi, tafiti zinaonesha kwamba, kila kitu tunachokutana nacho kwenye maisha yetu, kinachangia tabia zetu. Kuanzia jene tulizorithi, mazingira tunayoishi, familia, marafiki, biashara, matetemeko ya ardhi, shule, ajali, tv na redio, magazeti na chochote unachoweza kufikiria, kina mchango kwa hapo ulipo.
Hivyo unapotaka kujenga tabia nzuri za uongozi, angalia kwa umakini kila unachojihusisha nacho.
  1. Hakuna mtu anayeweza kukufundisha wewe kuwa wewe.
Wazazi wako wamekazana sana kukulea, jamii nayo imekazana kukufikisha hapo ulipo, lakini wote walifanya kazi moja, kujaribu kukufanya wewe uwe kama wengine. Ndiyo maana shuleni ulifundishwa vitu sawa na wengine, nyumbani ulikuwa unalinganishwa na wengine.
Ili kuwa kiongozi bora, lazima kwanza wewe uwe wewe, kitu ambacho hakuna mtu yeyote hapa duniani anaweza kukufundisha ila wewe. Wazazi wako hata kama wanakupenda kiasi gani, hawawezi kukufundisha wewe kuwa wewe, kwa sababu hata wao hawakujui wewe halisi ni yupi.
Hili ni jukumu kubwa ambalo wachache huweza kulikamilisha na kuweza kuwa viongozi bora.
  1. Viongozi bora wanaijua dunia inayowazunguka.
Ili kuwa kiongozi bora, lazima uweze kuijua dunia inayokuzunguka kama unavyojijua wewe mwenyewe. Lazima uwajue watu na mazingira tofauti na yale uliyozoea wewe. Katika kuijua dunia inayokuzunguka, unahitaji elimu pana na endelevu, kusafiri maeneo mbalimbali, kuwa na marafiki wa aina mbalimbali.
Ijue dunia zaidi ya hapo ulipo, hii itakuwezesha kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya.
  1. Aina tatu za kujifunza kwenye uongozi.
Katika kujifunza zipo aina tatu;
Aina ya kwanza ni kujifunza kuendelea na kile ambacho watu wamezoea kufanya, hapa mambo yanakuwa yale yale.
Aina ya pili ni kujifunza kutokana na mabadiliko yanayotokea. Hapa mabadiliko yanatokea na kuvuruga mambo, watu wanachukua hatua ili kuokoa hali isiwe mbaya.
Aina ya tatu ni kujifunza kwa ubunifu, hapa watu wanajifunza ili kuwa bora zaidi kila siku.
Katika aina hizi tatu, aina ya tatu ndiyo wanaitumia viongozi bora na inawawezesha kuwa mbele ya mabadiliko.
  1. Kusafiri kunakufanya ujijue na kuijua dunia vizuri.
Unaposafiri unavuruga yale mazoea ambayo umeshayajenga kwenye maisha yako ya kila siku. Hivyo kila unachofanya unapokuwa safarini, kinakuhitaji uwe makini sana ili usikosee au kupotea. Hali hii inakufanya utumie akili yako haswa badala ya kufanya kwa mazoea.
Kwa njia hii unajijua vizuri wewe mwenyewe na hata kuijua dunia pia, kwa kujua watu wa makabila na asili tofauti na namna wanavyoendesha maisha yao.
Mara zote nimekuwa nasema dunia ya sasa inatutaka sisi wote kuwa viongozi, kwa kuanzia kwenye familia yako, bila kuwa kiongozi, familia haiwezi kusimama, ukienda kwenye biashara, ili iwe na mafanikio, lazima uwe kiongozi mzuri.
Zingatia sana misingi hii tuliyojifunza kupitia uchambuzi huu wa kitabu, na pia nakusihi sana usome kitabu hichi, kwani yapo mengi mazuri.

MAABARA YA KISASA ZAIDI AFRIKA KUJENGWA TANZANIA

Tanzania Kujengwa Maabara ya kisasa ya Afrika
14 hours ago
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara ya Teknolojia ya Nyuklia kwenye Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC) Arusha, maaabara ambayo inatarajiwa kuwa ya kisasa kwa vifaa Afrika.

Akizungumza na viongozi mbali mbali wa mkoa huo na watumishi wa taasisi hiyo, Waziri Ndalichako amesema maabara hiyo ni ya watanzania na hivyo watumishi wanaofanya kazi katika tume hiyo  wasifanye kazi kwa ubinafsi na badala yake watangulize maslahi ya Taifa mbele.

Majengo ya maabara hiyo ya kisasa yanatarajiwa kukamilika Februari Mwaka 2018 ambapo yatagharimu kiasi cha shilingi   Bilioni 2.3, na ikikamilika Umoja wa Ulaya itafunga vifaa vyenye thamani ya Sh. Bilioni 11 ambapo  tayari baadhi ya vifaa vya Sh. Bilioni 2.6 vimekwishawasili nchini.

Pia Waziri na viongozi wengine wa Wizara wametembela Chuo cha Veta sehemu ya kuzalishia umeme kikuletwa pamoja na Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, kwa lengo la kukagua miundombinu ya chuo hicho pamoja kujionea vifaa vya kufundishia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Viongozi wengine ambao waliambatana na waziri kwenye ziara hiyo ni pamoja na Naibu waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia  Mhandisi Stella Manyanya na Naibu Katibu Mkuu, Profesa Saimon Msanjila

Wednesday, 23 August 2017

AJALI YAUA WATATU MOROGORO

Breaking News: Ajali ya treni na Coaster yaua wanafunzi Morogoro
12 minutes ago
WANAFUNZI watatu wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya basi la abiria aina ya Coaster lililobeba wanafunzi na raia kugonga treni katika eneo la TANESCO, Morogoro Mjini.

Taarifa za awali zimeeleza kuwa ajali hiyo imetokea leo alfajiri ambapo Coaster lilikuwa limebeba wanafunzi wengi wa Shule ya Sekondari ya Kayenzi waliokuwa wakienda shuleni pamoja na raia wachache lilipokatiza kwenye njia ya treni na kuligonga.

Imeelezwa pia kuwa treni lililiibuiruza Coaster hiyo kwa umbali wa mita 30 kabla ya kusimama hivyo kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

MAMBO YA KUFANYA UONDOKANE NA KUAJIRIWA

Watu wengi sana wanatamani kuwa na uwezo na uhakika wa kustaafu mapema, lakini ni wachache sana wanachukua hatua mahususi kuhakikisha wanalitimiza jambo hilo.
Ili uweze kustaafu mapema, mambo matatu yanahitajika: kipato cha uhakika, kuweka akiba na kuwekeza akiba yako.
Jambo la kuzingatia ili utimize lengo hili ni kufanya mambo hayo matatu yawe ndio kipaumbele chako maishani.
wekeza
Vijana wanajulikana kwa kuwa na tabia ya kutopenda kufata sheria, na linapokuja swala la matumizi ya pesa zao wanazozipata kwa jasho lao – wengi zaidi huwa hawataki hata ushauri kabisa.

Lakini uwezekano wa kustaafu mapema unaweza kuwafanya wengi washawishike kuachana na ubishi wao na kufikiria uhakika wa maisha yao ya uzeeni na kuanza kuchukua hatua za uhakika kuyanyoosha wangali bado vijana na wenye nguvu za kufanya kazi.

Zifuatazo ni njia hizo na jinsi ya kufanya:

1. Tengeneza chanzo imara cha mapato

Kama huna chanzo cha mapato, hutakuwa na nafasi hata ya kuanza kujenga utajiri. Hatua ya kwanza kabisa ya kuhakikisha unapata uhuru wa kipato ni kuwa na chanzo cha uhakika cha kipato ili uwe na uhakika kwamba kutokana na kipato hicho, unaweza kuweka akiba pamoja na kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Kwa baadhi ya watu, hii yaweza kumaanisha ufanye kazi kwa ufanisi kwenye ajira yako ya sasa ili uweze kutimiza lengo hili. Ukiwa na chanzo cha uhakika cha mapato, hata ikiwa ni kutokana na kazi za mkataba au tenda za kulipwa kwa siku, bado unaweza kuweka mipango ya baadaye na kuanza kuitekeleza, japo kidogo kidogo.

2. Weka akiba sehemu kubwa ya kipato hicho

Ukishakuwa na kipato cha uhakika, jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa hutumii pesa yote unayopata. Kujifunza jinsi ya kuishi maisha ya gharama nafuu chini ya kipato chako ni muhimu ili uweze kubaki na pesa (hasa ukianzia ujanani mwako) na uweze kujiwekea akiba itakayokusaidia kwa maisha yako yote yaliyobaki.

kwanza, miongoni mwa njia rahisi zaidi za kuhakikisha utakuwa na fedha uzeeni mwako ni kujiunga na mfuko wa hifadhi za kijamii. Mifuko hii itakusaidia kutoa michango yako kila mwisho wa mwezi au kwa muda maalum na kuja kuipata utakapotimiza umri wako wa kustaafu. Kwa waajiriwa, michango hii huwa inakatwa moja kwa moja kutoka kwenye mshahara wako – kwahiyo huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu hilo – lakini kwa ambao hawajaajiriwa, unaweza kujiunga kwenye mifuko hii kama mtu binafsi, kwakuwa inaruhusiwa kufanya hivyo pia. Michango unayoiweka ni kiasi kidogo sana cha pesa kwa mwezi, lakini faida yake uzeeni ni kubwa.

Pia, unaweza kupunguza matumizi yako ya pesa kwa kupunguza gharama za nyumba (kama umepanga) ili kodi yako kwa mwezi isizidi asilimia 30 ya kipato chako.

3. Wekeza akiba yako kwenye vitega uchumi vitakavyoongezeka au kutopungua thamani

Kuwa na pesa nyingi kwenye akiba yako ni jambo zuri, lakini unapoiwekeza pesa hiyo yaweza kusababisha tofauti kubwa sana kwenye safari yako ya kustaafu mapema.

Kuna wanaoamua kuwekeza kwenye sekta ya majumba, na inaweza ukunufaisha kwakuwa una uwezekano wa kuingiza kipato cha kila mwezi kutokana na kodi za pango.

Kwa wale wasiovutiwa na biashara ya majumba, unaweza kujifunza na kuwekeza kwa kununua hisa za makampuni mbalimbali ambayo yana rekodi nzuri ya ukuaji.

Mwanzo wa safari ya mafanikio ya kuwa na uhuru wa kipato unaanza kwa uamuzi wako kwamba kufanya hivyo ni muhimu sana kwako. Kisha ukiwa unazingatia malengo yako, basi unaweza kutimiza kila unachokitaka bila wasiwasi.

ANDAA SUPU YAKO YA MAWE LEO!!!!

Habari za leo rafiki yangu, 
Karibu kwenye makala yetu ya leo, ambapo kupitia makala hizi tunashirikishana maarifa muhimu ya kutuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.
Watu wengi wamekuwa wakitaka kuingia kwenye biashara, lakini kikwazo chao kikubwa kimekuwa waanzie wapi. Wengi wanakuwa hawana mtaji wa kuanza biashara, licha ya kuwa na mawazo bora ya kibiashara. Wengi wamekuwa hawapo tayari kuanzia chini, na hivyo kutafuta njia ya kuwawezesha kufika malengo yao makubwa kibiashara haraka, kitu ambacho huwa hakitokei na hivyo kuwaangusha zaidi.
Leo nakwenda kukushirikisha hadithi moja kuhusu supu ya mawe, ambayo itakuonesha ni jinsi gani unaweza kutoka hapo ulipo na kupiga hatua kubwa.
Hadithi hii nimekutana nayo kwenye mtandao, ina vyanzo mbalimbali, lakini hapa nitakushirikisha kwa namna ambavyo itakusaidia wewe kuchukua hatua.
Hadithi inakwenda kwamba kwenye kijiji kimoja, mwanakijiji aliona wanajeshi watatu wakiingia kijijini, walionekana kuchoka na wenye njaa. Mwanakijiji yule alikimbia na kuwaambia watu wengine kuna wanajeshi wanavamia kijiji, hivyo wote wakimbie na kujifungia ndani na kulinda vyakula vyao. Wanakijiji wote walifanya hivyo.
Wanajeshi wale walipoingia kijijini, wakiwa na njaa kweli, walijaribu kupiga hodi kwenye kila nyumba wakiomba kupata chakula. Mwanakijiji wa kwanza aliwaambia yeye hana hata chakula chake binafsi, wa pili akawaambia chakula chake kimeisha. Walienda nyumba kadhaa na kote majibu yakawa ni hakuna chakula.
Wakiwa wanafikiria wafanye nini, mmoja akawaambia wenzake kwamba ana wazo, akawaambia tutengeneze supu ya mawe. Basi wakapiga hodi kwa mwanakijiji mmoja, wakamwambia wanaomba chungu na kuni ili waandae supu ya mawe. Mwanakijiji yule kwanza alishangaa, supu ya mawe! Akajiambia kimoyomoyo, ngoja niwape nione hiyo supu ya mawe inakuwaje.
Basi walipewa chungu na kuni, wakawasha moto, wakachukua mawe matatu pamoja na maji wakayasafisha, wakaweka kwenye chungu, wakafunika na kukaa kusubiri supu iive. Basi habari zilianza kusambaa kijiji kizima, kwamba kuna wanajeshi wanaandaa supu ya mawe. Kwa kuwa lilikuwa jambo ambalo halijazoeleka, wasi wanakijiji walijikusanya pale kushuhudia supu hiyo ya mawe inakuwaje.
Wakiwa wamekaa pale, mwanajeshi mmoja akasema, supu hii ingekuwa tamu sana kama tungepata viazi, supu na viazi vinaendana sana. Mwanakijiji mmoja akasema ninavyo viazi, ngoja nikachukue. Mwanajeshi mwingine pia akasema tukipata karoti na hoho, supu hii itakuwa tamu zaidi, wanakijiji wengine wakaenda kuchukua karoti na hoho. Baada ya muda mfupi, kila mwanakijiji alijikuta anatoka na kwenda kuleta kiungo ambacho kitaifanya supu kuwa tamu zaidi. Supu ile ilipata kila aina ya kiungo.
Baadaye wanajeshi wale walisema supu imeshakuwa tayari, leteni vyombo tule, na kweli supu ile ilikuwa tamu sana, na kila mwanakijiji akasema supu ya mawe ni tamu mno.
Kitu ambacho hawakujua ni kwamba, yale mawe hayajachangia chochote kwenye supu, bali viungo ambavyo kila mmoja amechangia, ndiyo vimefanya supu iwe tamu.
Je unawezaje kuitumia hadithi hii kwenye maisha yako?
Kama umenifuatilia vizuri tangu mwanzo utakuwa umeshaanza kuona jinsi ya kutumia hadithi hii. Unaweza kuitafsiri vyovyote utakavyo, lakini mimi nitaitafsiri na kukufundisha kitu kikubwa sana kwenye kuanza biashara.
Utakapokuwa na wazo kubwa la kibiashara, ukitegemea wengine wakusaidia kulifanyia kazi, kila utakayemwomba akusaidia atakuambia hana fedha. Wengine watakuambia maisha ni magumu, wengine watakuambia kwa sasa hawapo vizuri. Siyo kwamba kweli hawana fedha, ila wana hofu kwamba fedha zao zitapotea. Kama ilivyokuwa kwa wanakijiji, walikuwa na hofu kwamba wale wanajeshi wangeipa chakula chao chote.
Lakini unapochagua kuanza na kile ulichonacho, kuanza na wazo lako kubwa, kuweka nguvu na juhudi kubwa pale unapoanzia, kuonesha mapenzi makubwa kwenye kile unachofanya, hapa watu wataanza kukufuatilia, kukuangalia waone unaelekea wapi. Hii ndiyo supu yako ya mawe.
Watu wakishaanza kukuangalia sasa, na kukufuatilia unaelekea wapi, hapo sasa ndipo unaweza kuwashawishi wakaweka mtaji zaidi, wakakusaidia rasilimali ulizokosa, wakakuunganisha na watu unaowahitaji ila hawakujui na unaweza kuwajua kupitia wao. Utapata kila aina ya msaada kwa sababu unaonekana kuna kitu unafanya.
Mwishoni biashara inakuwa na mafanikio na kila mtu anasema umeweza kukuza biashara kubwa, wengi wasijue kuna michango ya wengi imekufikisha pale.
Unahitaji kuwa na supu ya mawe ambayo unaiandaa, supu hii ya mawe ni kile kilichopo ndani yako, ambacho kwa nje kinaonekana hakiwezekani, lakini wewe upo tayari kupambana kuhakikisha kinawezekana. Supu hii ya mawe ni kuamini kwako kwenye lile wazo ulilonalo, kuwa na ndoto kubwa, kuwa na mapenzi makubwa mno kwenye ile biashara unayowaambia watu unataka kufanya. Pia kuweza kuanzia pale ulipo, kuweka kazi kubwa zaidi ya wengine. Kila mtu anapokuona kwenye hali hiyo, anakuwa tayari kuleta mawazo bora zaidi, fedha, watu na mengine unayohitaji ili kukamilisha biashara yako.
Nimekuwa nasema mara zote, kusema tu una wazo la biashara hakutawafanya watu wahangaike na wewe, wapo wengi mno wenye mawazo, ila pale unapochukua hatua na watu wakaanza kuona kumbe kweli unamaanisha, watajileta wenyewe kukusaidia.
Swali langu kwako rafiki yangu ni moja tu; SUPU YAKO YA MAWE NI NINI?
Jipe jibu la swali hili, na kama hujaanza kuiandaa supu hiyo, chukua chungu na kuni, kisha anza kupika supu yako ya mawe. Watu watakufuata pale ambapo kuna kitu unafanya, watakukataa pale unapokuwa na maneno pekee, kama tulivyoona kwa wanajeshi kwenye hadithi hii.

TAMBO ZA YANGA BHANAA

Yanga yatamba kuanza kuhesabu makombe leo
58 minutes ago
BENCHI la Ufundi la Yanga, limesema kuwa leo Jumatano linaanza kuhesabu makombe ya msimu wa 2017/18 kutokana na kuwa na uhakika wa kuifunga Simba.

Leo Jumatano katika Uwanja wa Taifa jijini Dar, Yanga itapambana na Simba ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa msimu wa 2017/18.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, amesema kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kisiwani Pemba, wana uhakika wa kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao, Simba.

“Mechi yetu na Simba tuna uhakika wa kushinda kutokana na maandalizi tuliyoyafanya, tumejiandaa tayari kwa kuanza kuhesabu makombe msimu wa 2017/18, hakuna mtu wa kuzuia jambo hilo.

“Benchi la ufundi chini ya kocha George Lwandamina, limetuhakikishia kwamba wachezaji wote waliokwenda kambini Pemba wapo vizuri kiafya tayari kucheza mechi hiyo, inafahamika tangu zamani kwamba Obrey Chirwa, Geofrey Mwashiuya na Benno Kakolanya watakosekana kutokana na majeraha mbalimbali waliyonayo,” alisema Ten.

your dream job

Nafasi za kazi leo Agosti 23
22 minutes ago
Bonyeza Links Zifuatazo Kusoma zaidi na Kuapply

6 Jobs Opportunities at NMB Tanzania

Job Opportunity at Vodacom Tanzania

Job Opportunity at Qatar Airways, Reservation & Ticketing Supervisor

Job Opportunities at Mwananchi Communication Limited

Job Opportunity at Standard Bank, Officer, Credit Risk Management

Job Opportunity at Standard Bank, Officer, Accounts Payable

Job Opportunity at Palladium Group (Tanzania) Limited, Program Manager

Job Opportunity at Sunda Investment Co Limited, Customer Service Supervisor

Nafasi zaidi Ingia www.ajirayako.co.tz