Thursday, 24 August 2017

MATUMIZI SAHIHI YA MANENO HAPANA,NDIYO NA LABDA

Leo tunakwenda kuangalia maneno matatu muhimu, ambayo huwa tunayatumia kirahisi, lakini madhara yake ni makubwa. Tukijua namna sahihi ya kutumia maneno haya, tutaweza kufanya mapinduzi makubwa sana kwenye maisha yetu.
Maneno tunayokwenda kuyaangalia leo ni NDIYO, HAPANA na LABDA.
Haya ni maneno ambayo yanahusiana moja kwa moja na matumizi ya muda wetu. Kuna namna sahihi ya kutumia maneno haya ambayo inatuwezesha kuwa na muda wa kutosha kufanya mambo muhimu kwetu. Pia ipo namna ambayo siyo sahihi ya kutumia maneno haya, na inatupelekea kupoteza muda mwingi kwenye maisha yetu.
Neno NDIYO.
Hili ni neno ambalo tumekuwa tunalitumia vibaya kwenye maisha yetu, ni neno moja ambalo limekuwa linapoteza muda wetu kuliko maneno mengine yoyote.
Kwa mfano umepanga kwamba kila siku jioni unapomaliza kazi zako, utakuwa unasoma kitabu ili kuongeza maarifa zaidi ya kile unachofanya. Umefika muda na umekaa kuanza kusoma kitabu chako, mara inaingia simu ya rafiki yako, anakuambia yupo sehemu fulani na marafiki wengine, na wanakuulizia. Wewe unasemaje, NDIYO, nakuja. Na unajipa sababu kabisa kwamba nisipoenda watanichukuliaje, hichi kitabu naweza kukisoma muda wowote tu.
Hilo ni moja, lakini yapo mengi sana tunayosema ndiyo ambayo yanatupotezea muda wetu. Mambo kama simu, ujumbe wa simu, mitandao ya kijamii, habari, umbeya na mengine mengi, tunaposema ndiyo kuyafuatilia, maana yake tunahamisha matumizi ya muda wetu. Tunaacha kufanya yale ambayo ni muhimu sana kwetu, na kuishia kufanya yale ambayo siyo muhimu.
Watu wengi husema ndiyo kwa sababu wanaogopa kusema hapana. Wanaona wakisema hapana wanawaumiza wengine na hivyo kukubali ili tu kuwaridhisha. Na nataka nikuambie leo rafiki yangu, hakuna sababu ya hovyo ya kusema ndiyo kama hiyo. Na ni kwa sababu zifuatazo;
Moja; unaposema ndiyo kwenye mambo ya wengine, maana yake unasema hapana kwenye mambo yako binafsi. Hivyo kama unawaridhisha wengine, jua kabisa kwamba unajiangusha wewe mwenyewe.
Mbili; hakuna anayejali kuhusu wewe kama unavyofikiria. Usidhani kwamba watu muda wote wanafikiri kuhusu wewe pekee na namna umewakatalia kuhusu kitu fulani, watu wanaendelea na maisha yao.
Tatu; kusema ndiyo kwa sababu unaogopa kusema hapana, hakutakuacha salama. Kwa sababu hutakamilisha ndiyo ile kama ulivyoahidi na hapo utaharibu zaidi mahusiano yako na wale uliowaambia ndiyo. Unajua ni bora useme hapana watu watafute wengine wanaoweza kufanya, kuliko useme ndiyo halafu uanze kuwazungusha.
Neno HAPANA.
Hili ndiyo neno lenye uhuru kwako na maisha yako. Unaposema hapana, unajijengea uhuru, unajipa muda wa kufanya yale ambayo ni muhimu kwa maisha yako. Unaposema hapana, unajipa nafasi ya kuendesha maisha yako vile unavyotaka wewe.
Lakini neno hapana ni neno ambalo wengi wana hofu ya kulitumia. Wengi huona ni vibaya na kuona wengine watawachukulia vibaya, au wataonekana wana dharau kwa kusema hapana.
Na hapa ndipo sanaa inapohitajika, haimaanishi mtu akuombe kufanya kitu halafu umwambie HAPANA siwezi kufanya. Zipo njia nyingi za kusema hapana bila ya kuwaumiza wengine, lakini hapana ikawa imefika.
Kwa mfano mtu amekuomba uhudhurie kikao cha harusi, ambacho unajua hakuna kitu kikubwa mnakwenda kufanya pale, kwa sehemu kubwa ni kuongea mambo yale yale ambayo yamekuwa yanaongelewa, labda kukusanya michango. Unaweza kumwambia nashukuru sana kwa nafasi hii ya kushiriki kikao hicho, lakini kwa wakati huo wa kikao nina jambo jingine nafanyia kazi, nawatakia kila la kheri na kikao kiende vizuri.
Kwa vyovyote vile, hakikisha unasema hapana, na unaisema kwa namna ambayo mtu ataona ni sawa.
Je ni mambo gani useme hapana?
Kwako binafsi; jambo lolote ambalo halichangii wewe kufikia ndoto za maisha yako, sema hapana. Sema hapana kwa habari, udaku, majungu, umbeya, mitandao ya kijamii, uvivu na kufuatilia maisha ya wengine.
Kwa wengine; chochote ambacho mtu anataka ufanye, ambacho siyo muhimu sana kufanyika kwa wakati huo, na kinakuzuia wewe kufanya makubwa ziadi, sema hapana.
Neno LABDA.
Hili ni neno la hovyo kabisa, na usilitumie kabisa. Lifute kabisa kwenye orodha ya maneno unayotumia.
Watu wamekuwa wakitumia neno labda ili kukaa katikati ya ndiyo na hapana. Wanakuwa wanataka kusema hapana, lakini wanaogopa, na wakati huo hawapo tayari kusema ndiyo, hivyo wanasema labda.
Kutumia neno labda kutakuharibia mambo mengi kuliko unavyofikiri. Watu watakuchukulia kama mtu usiye na msimamo na usiyeeleweka. Kusema labda kunawafanya watu washindwe kujua unasimama wapi na wategemee nini kwako.
Sema NDIYO kwenye yale mambo muhimu, sema HAPANA kwa mambo ambayo siyo muhimu na kamwe usitumie neno LABDA.
Fanyia kazi haya rafiki, na matumizi ya muda wako yatakuwa bora sana.

No comments:

Post a Comment